Van Gaal aamini Man Utd watajinasua

Leicester Haki miliki ya picha PA
Image caption Manchester United wamo alama tisa nyuma ya viongozi wa ligi Leicester City

Louis van Gaal amesema Manchester United wanaweza wakaimarika lakini lazima waboreshe uchezaji wao mara moja.

Meneja huyo aliondoka ghafla kwenye kikao cha wanahabari Jumatano baada ya kuwahutubia kwa dakika tano pekee.

United wameenda mechi sita bila kushinda mechi hata moja, wakichapwa mechi tatu mfululizo, na Van Gaal amesema anapitia kipindi kigumu zaidi Old Trafford.

“Hatuwezi kuficha ukweli huu, kwamba tunapitia kipindi kibaya sana. Mambo lazima yaanze kuimarika mara moja.”

Van Gaal alisema hayo kwenye tathmini yake ya mechi kati ya United na Chelsea itakayochezwa 28 Desemba.

Aliyekuwa meneja wa Chelsea Jose Mourinho, aliyefutwa kazi majuzi, ni mmoja wa wale ambao ripoti zinasema wanaweza wakamrithi Van Gaal.

"Tunaweza kubadilisha mambo. Njia bora zaidi ya kujitoa katika kipindi hiki na kuimarika ni kukaa sote pamoja,” alisema.

Red Devils kwa sasa wamo nambari sita ligini, alama tisa nyuma ya viongozi Leicester City baada ya kuchapwa 2-0 na Stoke City.

Walizomewa na mashabiki baada ya kushindwa 2-1 na Norwich Jumamosi.

Mashabiki wanataka timu yao icheze mchezo wa kushambulia zaidi.