Chipukizi wa Chelsea akataa kukaa Crystal Palace

Bamford Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bamford hajaanza mechi haja moja Ligi ya Premia akiwa Palace

Mshambuliaji wa Chelsea Patrick Bamford amesema amekatiza kipindi chake cha kuwa Crystal Palace kwa mkopo wa msimu mmoja.

Bamford, 22, ametangaza uamuzi wa kurejea Chelsea kabla ya mkopo wake kumalizika baada ya klabu hiyo kutoka sare ya 0-0 na Swansea Jumatatu.

Imebainika tayari alikuwa amemjulisha meneja wake Alan Pardew.

"Hiyo ilikuwa mechi yangu ya mwisho Palace,” alisema. “Kusema kweli, kimekuwa kipindi kibaya. Hakuna mchezaji apendaye kukaa benchi bila kuchezeshwa.

“Huo ulikuwa uamuzi wangu. Bosi wangu hajazungumza nami.”

Bamford, anayechezea timu ya taifa ya England ya wachezaji wa umri wa chini ya miaka 21, hajaacha kwenye mechi yoyote Ligi ya Premia tangu awasili Palace kutoka Chelsea.

Amecheza mechi tano ligini kama nguvu mpya.

Mechi pekee mbili alizoanza kikosini zilikuwa za Kombe la Ligi.

Bamford alipoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya kuingia kama nguvu mpya dhidi ya Swansea Jumatatu. Aligonga mpira kuelekea kwa kipa Lukasz Fabianski akiwa hatua 12 kutoka kwenye goli.