Twitter yamponza Sergi Guardiola Barcelona

Barca Haki miliki ya picha Getty
Image caption Guardiola, 24, alikuwa amejiunga na klabu ya akiba ya Barcelona

Huwa ndoto ya wachezaji kujiunga na Barcelona lakini mchezaji moja ametimuliwa muda mfupi tu baada ya kujiunga na klabu hiyo, kutokana na mtandao wa kijami.

Mshambuliaji Sergi Guardiola alikuwa ametia saini mkataba wa kujiunga na timu ya akiba ya Barcelona.

Lakini saa chache baadaye, maafisa wa klabu walijulishwa kuhusu “jumbe za kuudhi kwenye Twitter” ambazo aliziandika miaka miwili iliyopita kuhusu Barca na jimbo la Catalona.

Guardiola, 24, aijiunga na Barcelona B Jumatatu, lakini kwa mujibu wa gazeti la michezo la Uhispania la Marca, mkataba wake ulibatilishwa klabu ilipogundua alikuwa ameandika jumbe za kuunga mkono mahasimu wakuu wa Barcelona Real Madrid kwenye Twitter.

Aidha, alikuwa ametumia lugha ya kuudhi dhidi ya wakazi wa Catalona, jimbo linalopigania kujitenga kutoka kwa Uhispania.

Guardiola alianza msimu huu akichezea klabu ya Alcorcon ya jiji la Madrid ambayo imekuwa ikicheza ligi ya daraja la pili Uhispania.