Real Madrid wapoteza rufaa Copa del Rey

Cheryshev Haki miliki ya picha Getty
Image caption Cheryshev hakufaa kuchezea Real dhidi ya Cadiz

Real Madrid wamepoteza rufaa yao dhidi ya uamuzi wa shirikisho la soka la Uhispania wa kuwaondoa michuano ya Copa del Rey kwa kumchezesha mchezaji asiyefaa.

Mabingwa hao mara 19 waliadhibiwa kwa kumchezesha winga Denis Cheryshev dhidi ya Cadiz hatua ya 32 bora mnamo 2 Desemba.

Cheryshev alifaa kuwa akitumikia marufuku ya mechi moja kutokana na kadi za manjano alizoonyeshwa akichezea Villarreal kwa mkopo.

Mahakama ya kutatua mizozo ya kimichezo nchini Uhispania ilitupilia mbali rufaa ya Real baada ya “kutathmini taarifa za pande zote”.

Klabu hiyo bado inaweza kukata rufaa lakini itahitajika sasa kwenda kwa mahakama za kawaida.

Real, ambao wamo nambari tatu katika La Liga nyuma ya Barcelona na Atletico Madrid, walishinda Copa del Rey mara ya mwisho 2014.