Sadio Mane aachwa nje kwa kuchelewa

Mane Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Ilikuwa mara ya pili kwa Sadio Mane kuchelewa

Meneja wa Southampton Ronald Koeman amesema alimuweka nyota Sadio Mane kwenye benchi kwa sababu ya kuchelewa kufika kwa kikao cha kabla ya mechi.

Kiungo huyo wa kati wa Senegal aliwekwa kwenye benchi mechi ambayo klabu yake ililazwa 1-0 na Norwich Jumamosi, na alichezeshwa dakika 10 za mwisho pekee.

"Ni lazima uwaheshimu wachezaji wenzako, na mashabiki na klabu kwa sababu huwa inalipia pesa nyingi,” Koeman aliambia BBC Sport.

"Kunilazimisha kubadilisha kikosi saa mbili kabla ya mechi ni jambo lisilokubalika."

Sadio Mane, 23, alijiunga na klabu hiyo kutoka Red Bull Salzburg mwaka 2014, na alikuwa amewachezea mechi zote 19 Ligi ya Premia msimu huu, na kuwafungia mabao mara tatu.

"Hii ni mara ya pili tukio kama hili kufanyika. Mwaka jana kuna wakati alichelewa kufika uwanjani na leo alichelewa kufika kikao cha kabla ya mechi,” Koeman ameongeza.

“Siwezi kuelewa ni vipi makosa ya aina hii yanaweza kutokea.”

Kando na kumkosa Mane, Southampton waliathiriwa pia na kufukuzwa uwanjani kwa Mkenya Victor Wanyama, dakika mbili kabla ya Alex Tettey kufungia Norwich bao la ushindi mechi hiyo ya Jumamosi.