Hiddink: Inawezekana Chelsea kumaliza nne bora

Chelsea Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chelsea kwa sasa wamo nambari 14 ligini

Kaimu meneja wa Chelsea Guus Hiddink amesema bado inawezekana klabu hiyo kumaliza katika nne bora Ligi ya Premia baada yao kulaza Crystal Palace 3-0 Jumapili.

Hata hivyo, amekiri kwamba ni jambo ngumu.

Klabu hiyo ya Stamford Bridge sasa imeenda mechi nne bila kushindwa, kwa mara ya kwanza msimu huu, na kupanda hadi nambari 14 ligini.

Hata hivyo, bado wanapungukiwa na alama 13 kufika eneo la kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Ushindi wao dhidi ya Palace, walio nambari saba ligini, uliibua matumaini kwamba huenda wakafanya vyema kipindi hiki cha pili cha msimu.

"Kila mmoja anajua kwamba tuna wachezaji stadi lakini wakati mwingine, timu baada ya kutawazwa mabingwa, hulegea,” alisema Mholanzi huyo.

“Nilipoanza, tulisema ikiwezekana tujipate nafasi ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya litakuwa jambo nzuri sana. Ni vigumu kwa sababu ligi imekuwa na ushindani sana. Kila timu inaweza kushinda nyingine. Hii inaifanya vigumu kufika huko (nne bora).

"Lakini tukiendelea kucheza kama leo tunaweza kuwa na furaha na tutaanza kupata matokeo mazuri. Bado inawezekana, ingawa bado kuna kibarua.”

Hiddink alipewa kazi ya ukufunzi baada ya Mreno Jose Mourinho kufutwa kazi mwezi jana.