Azam, Yanga sare Mapinduzi Cup

Mabingwa wa Tanzania Bara Timu ya Yanga imetoshana nguvu na Azam FC, kwa kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya Kundi B michuano ya Mapinduzi Cup 2016 iliyopigwa jana Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.

Azam FC ndio walitangulia kufunga kwa bao kupitia kwa Kipre Tchetche dakika ya 58 na Yanga kusawazisha bao hilo kupitia Vinceny Bosou dakika ya 82 kipindi cha pili.

Mpaka sasa matokeo haya yameacha kitendawili ni timu gani itafuzu nusu fainali toka Kundi B ingawa Yanga na Mtibwa Sugar wanaweza kupita wote wakitoka sare katika mechi yao ya mwisho ambayo wanakutana.

Ili kusonga hatua ya nusu fainali, Azam FC inapaswa kushinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Mafunzo FC.

Michuano hii itaendelea tena hii leo Jumatano Januari 6 kwa michezo miwili, ambapo Timu ya Jamhuri itaivaa JKU, na URA itachuana na Simba.