Wachezaji bingwa Afrika kutangazwa

Samatta Haki miliki ya picha CAF Online Twitter
Image caption Samatta alisaidia TP Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika 2015

Macho yote yameelekezwa mji wa Abuja nchini Nigeria ambapo baadaye leo wachezaji bora wa soka kutoka Afrika 2015 watatangazwa.

Makala ya 24 ya Tuzo hizo za Glo-CAF, zinazotolewa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF), yamekuwa na ushindani mkali kutoka kwa wachezaji wa soka wanaosakata soka ya kulipwa ndani na nje ya Afrika.

Orodha ndefu iliyowasilishwa mwezi Oktoba mwaka uliopita, ilipunguzwa hadi wachezaji watatu kila kitengo.

Matumaini ya Afrika mashariki yamo kwenye kitengo cha tuzo ya mchezaji bora anayechea soka barani Afrika ambapo mshambuliaji Mbwana Aly Samatta wa Tanzania na klabu ya TP Mazembe yumo ndani.

Nyota huyo aliyeisaidia klabu ya Mazembe kuondoka na kombe la klabu bingwa afrika, atakuwa anawania taji hilo dhidi ya mdakaji wa klabu yake ya Mazembe, Robert Kidiaba ambaye pia ni kipa wa DR Congo na raia wa Algeria Baghdad Bounedjah anayeichezea Etoile du Sahel.

Samatta aliibuka mfungaji mabao bora Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka uliopita.

Katika kitengo cha Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kinachoshirikisha wachezaji wa ligi za nje, Yaya Toure, aliyeshinda tuzo hiyo mara nne awali, ni mmoja wa wanaoipigania.

Toure, ambaye ni kiungo wa Ivory Coast na Manchester City anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mshambuliaji wa Gabon na klabu ya Borrussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang, na Andrew Ayew kutoka Ghana na Swansea City.

Tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo 1992, ni wachezaji kumi na wanne pekee wakiwemo Yaya Toure na Didier Drogba ambao wametuzwa.

Image caption Toure aliongoza Ivory Coast kutwaa ubingwa wa Afrika mapema 2015

Wanamuziki maarufu akiwemo Awilo Longomba, watatoa burudani katika hafla hiyo inayotarajiowa kuhudhuriwa na mamia ya wachezaji, wasimamizi na wapenzi wa soka.

Mchezaji bora wa kike pia atapatikana kati ya orodha inayojumuisha raia wa Cameroon Gabrielle Onguene na Gaelle Enganamouit, Ngozi Ebere wa Nigeria, N’rehy Tia Ines wa Cote d’Ivoire na Portia Boakye kutoka Ghana.

Wachezaji wa umri mdogo

 • Adama Traore - Mali,
 • Kelechi Nwakali - Nigeria,
 • Samuel Diarra - Mali,
 • Victor Osimhen - Nigeria
 • Yaw Yeboha - Ghana

Kocha Bora

 • Baye Ba –Mali
 • Emmanuel Amuneke – Nigeria
 • Fawzi Benzarti - Etoile Sportive de Sahel,
 • Herve Renard - Cote dIvoire
 • Patrice Carteron - TPMazembe

Wachezaji wanaoibuka

 • Azubuike Okechukwu - Nigeria,
 • Djigui Diarra - Mali
 • Etebo Oghenekaro - Nigeria,
 • Mahmoud Abdelmonem - Misri
 • Zinedine Ferhat - Algeria

Tuzo za wakongwe

 • Charles Kumi Gyamfi – Ghana
 • Samuel Mbappe Leppe - Cameroon

Timu Bora ya Taifa ya mwaka

 • Ivory Coast
 • Ghana
 • Mali U-17
 • Nigeria U-17
 • Nigeria U-23