Messi aing’arisha Barcelona

Messi Haki miliki ya picha AP
Image caption Messi alifungia Barca mabao mawili

Mshambuliaji wa klabu ya Barcelona Lionel Messi amekuwa shujaa baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Espanyol katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora michuano ya Kombe la Mfalme, maarufu kama Copa del Rey.

Mechi hiyo ilichezewa uwanja wa Nou Camp.

Katika ushindi wa mabao hayo manne wachezaji wengine walioiwezesha timu hiyo kushinda ni Gerard Pique na Neymar Da silva.

Bao pekee la Espanyol lilifungwa na Felipe Caicedo.

Espanyol walimaliza mechi hiyo wakiwa na wachezaji tisa uwanjani baada ya Arsensio Pérez na Diop kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kufuatia mabao hayo, Messi sasa amefikisha idadi ya mabao aliyofunga msimu huu, licha ya majeraha, hadi 14 kutoka kwa mechi 21.

Messi ni mmoja wa wanaoshindania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani ijulikanayo kama Ballon d'Or. Mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa Jumatatu wiki ijayo.