Rogasian Kaijage ajiuzulu Twiga Stars

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ya mpira wa miguu Twiga Stars, Rogasian Kaijage amejiuzulu nafasi.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limesema Kaijage aliwasilisha barua ya kujiuzulu akitaja majukumu mengine.

Kaijage aliiongoza Twiga Stars kwenye fainali za michezo ya Afrika (All Africa Games) zilizofanyika nchini Congo Brazzavile Septemba mwaka jana, baada ya kuiondoa timu ya taifa ya Zambia katika hatua ya mtoano.

Kocha huyo mwenye leseni A ya CAF amekuwa akizinoa timu za taifa za wanawake ya wakubwa Twiga Stars pamoja na timu ya wanawake wenye umri chini ya miaka ya 20 (Tanzanite) tangu mwaka 2013.

Aidha maandalizi ya mchezo kati ya Twiga Stars dhidi ya Zimbambwe yataendelea chini ya kocha atakayeteuliwa kuchukua nafasi yake, mchezo utakaochezwa mwezi Machi mwaka huu na mshindi kucheza na Zambia.