Wanariadha UK wataka rekodi za riadha kufutwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanariadha wa Urusi

Shirikisho la mchezo wa riadha nchini Uingereza, UK Athletics, UKA limependekeza kuwa rekodi zote za mchezo huo zibadilishwe upya ili kusaidia mwanzo mpya utakaohakikisha kumalizwa kwa utumizi wa madawa ya kusisimua misuli michezoni.

Shirikisho la mchezo huo duniani IAAF, limetoa mapendekezo kadhaa, ikiwemo kuwapiga marufuku kwa muda mrefu wanariadha watakaopatikana na hatia na pia kuwepo kwa sajili rasmi ya wanariadha waliopatikana na hatia.

Pendekezo hilo limetolewa kufuatia madai ya wakuu wa mchezo huo kuhusika na sakata ya kuficha na kuwalinda wanariadha watundu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mwanariadha wa Urusi aliyeshinda dhahabu.

Mwenyekiti wa UKA, Ed Warner amesema huu ni wakati wa kufanya mabadiliko makuu, akisema kuwa hadhi na heshima ya mchezo huo iliharibiwa sana mwaka wa 2015.

Katika miezi ya hivi karibuni, riadha duniani imekumbwa na dosari hasa kufuatia taarifa kadhaa kuhusu utumizi wa madawa ya kusisimua misuli.

Urusi, ambayo ni moja ya mataifa yenye wanariadha maarufu, imepigwa marufuku kushiriki katika mashindano ya kimataifa, baada ya serikali ya nchi hiyo kutuhumiwa kufadhili na kuhimiza wanariadha kutumia madawa hayo yaliyoharamishwa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Lamin Diack

Aliyekuwa rais wa shirikisho la mchezo huo duniani, IAAF, Lamine Diack, anachunguzwa baada ya madai kuwa alipokea hongo ili kutowaadhibu wanariadha wa Urussi. Diack hata hivyo amekanusha madai hayo.

Maafisa wengine wa tatu wa IAAF, akiwemo mwanawe Diack, Papa Massata Diack, walipigwa marufuku maishani, baada ya uchunguzi kubainisha kuwa walijaribu kumlaghai mwanariadha mmoja wa Urusi, aliyetuhumiwa kutumia madawa ya kusisimua misuli.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Lord Coe

Rais mpya wa IAAF, Lord Coe ameapa kuimarisha juhudi za kupambana na utumizi wa madawa michezoni, na pia amedokeza kuwa atabuni kitengo maalum kupambana na tatizo hilo kabla ya michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa mjini Rio mwaka huu.