Van Gaal: Tungefunga mabao sita Newcastle

Van Gaal Haki miliki ya picha PA
Image caption Van Gaal hakufurahishwa na uamuzi wa refa kuwapa Newcastle penalti

Meneja wa Manchester United Louis van Gaal amesema klabu yake ilikuwa na nafasi ya kufunga mabao sita mechi ambayo walitoka sare ya 3-3 ugenini Newcastle.

Van Gaal alikuwa Jumatatu amesema kwamba kuna wakati mwingine amekuwa hapendezwi na uchezaji wa timu yake lakini kwenye mechi hiyo walicheza vyema na nusura waondoke na ushindi lakini Paul Dummett akasawazishia wenyeji dakika za mwisho.

“Bila shaka ninahisi ni kama tulishindwa. Tulitupa ushindi,” alisema Mholanzi huyo ambaye vijana wake wakati mmoja waliongoza 2-0.

"Tungefunga mabao sita lakini lazima ufunge bao moja zaidi ya mpinzani wako.”

Uwanjani St James' Park, Manchester United walishambulia sana dakika za kwanza 45 na Wayne Rooney aliwafungia penalti na kisha akasaidia Jesse Lingard kufunga la pili.

Baada ya Newcastle kusawazisha kupitia Georginio Wijnaldum na Aleksandar Mitrovic, Rooney aliwarejesha tena mbele lakini Lingard na Marouane Fellaini walipoteza nafasi murua za kufunga kabla ya Dummett kusawazisha.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rooney alifungia Manchester United mabao mawili

“Tulitupa ushindi, nimewaambia hivyo wachezaji wangu,” Van Gaal ameongeza.

Pia alikosoa uamuzi wa refa wa kutoa penalti baada ya Chris Smalling kudaiwa kumchezea vibaya Mitrovic, penalti ambayo mshambuliaji huyo alifunga na kusawazisha.

"Refa alitoa penalti na hakukuwa na kosa lolote, ni wachezaji wawili walikuwa wanakabiliana, na huwezi kuamua ni nani amemfanyia mwingine madhambi.”