CHAN: Nigeria wawazidi nguvu Niger

Niger
Image caption Mabao yote yalifungwa kipindi cha pili

Nigeria walichapa majirani wao 4-1 kwenye mechi ya taifa bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani iliyochezewa uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali.

Moses Okoro aliifungia Nigeria goli la kwanza kwenye dakika ya 46.

Niger ilionekana kutoa upinzani mkali kabla ya kuishiwa nguvu na kusalimu amri mikononi mwa Super Eagles.

Elvis Chisom Chikatara, aliyeingia kama nguvu mpya dakika ya 57 alifunga magoli hayo mengine matatu.

Bao la kufutia machozi la Niger lilifungwa na Adje Zakari Adebayor.

Katika mechi iliyochezwa mapema, Tunisia ilitoka sare na Guinea kwa kufungana magoli mawili.

Magoli ya Tunisia yalipachikwa kimiani na mshambuliaji wao Ahmed Akaichi (32) na dakika ya 51.

Upande wa Guinea pia mshambuliaji wao Camara Agogo alinusa nyavu mara mbili, dakika ya 40 na goli la pili kunako dakika ya 83.

Leo, Zimbabwe na Zambia zitashuka dimbani Rubavu katika kundi D na baadaye Mali wakutane na Uganda.