Javier Mascherano kortini kuzuia kutupwa jela

Javier Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mascherano alikuwa amekiri makosa mawili ya kukwepa kufichua mapato yake

Difenda wa Barcelona na Argentina Javier Mascherano amefika mahakamani kujaribu kuzuia asitupwe jela kwa kosa la ulaghai katika ulipaji ushuru.

Anadaiwa kutumia ulaghai kukwepa kulipa ushuru wa jumla ya euro1.5m (£1.1m).

Mascherano, 31, awali alikiri makosa mawili ya kukosa kutangaza mapato yake kamili ya 2011 na 2012.

Jaji atatoa uamuazi wa iwapo Mascherano anaweza kulipa faini ya juu ili asifungwe jela, kwa mujibu wa ripoti Uhispania.

Anadaiwa kujaribu kutumia hila kuficha mapato kutoka kwa uuzaji wa haki za kutumia picha zake akitumia kampuni anazomiliki ng’ambo.

Stakabadhi za mahakama zinaonyesha mchezaji huyo alilipa jumla ya euro 1.75m, kiasi kamili alichodaiwa pamoja na riba.

Baada ya kufika kortini Catalonia, nyota huyo wa zamani wa Liverpool na West Ham aliandika kwenye Twitter: “Mimi ni mchezaji soka ya kulipwa, sifahamu sana masuala ya ushuru na sheria.

“Kuangazia masuala hayo magumu, mimi huwategemea watu wengine.

“Katika maisha yangu ya uchezaji, nimekuwa mtu mwaminifu, wa kuwajibika na anayeheshimu wachezaji wengine na klabu ambazo nimechezea.”