Man Utd wakana kukutana na Guardiola

Pep Haki miliki ya picha All SPort
Image caption Guardiola ataondoka Bayern baada ya kumalizika kwa msimu huu

Manchester United wamekanusha habari kwamba walikutana na kuzungumza na meneja wa Bayern Munich Pep Guardiola kuhusu uwezekano wake kuwa meneja wao.

Tovuti ya France Football ilikuwa imesema mkutano huo ulifanyika mjini Paris lakini United wamesema habari hizo si za kweli.

Meneja wa sasa wa United Louis van Gaal amekabiliwa na shinikizo baada ya klabu hiyo kutofanya vyema ligini Uingereza na Ulaya..

Guardiola, 45, anataondoka Bayern Munich majira yajayo ya joto na amesema amepokea maombi kutoka kwa klabu kadha za Uingereza.

Manchester City wamo kwenye nafasi nzuri ya kumchukua, lakini Chelsea na United wamedaiwa kumtafuta pia.

Bayern Munich walikuwa kwenye kambi ya mazoezi Doha wakati wa mapumziko ya msimu wa baridi na watarejea kucheza Ijumaa dhidi ya Hamburg.