Chelsea wapewa Man City katika FA

City Haki miliki ya picha AP
Image caption Mechi zitachezwa wikendi ya 19-22 Februari

Chelsea watacheza nyumbani dhidi ya Manchester City katika raundi ya tano ya Kombe la FA.

Klabu ya League One Shrewsbury Town, iliyoorodheshwa ya chini zaidi miongoni mwa timu zilizosalia kwenye shindano hilo nayo itakuwa mwenyeji wa Manchester United katika uwanja wa New Meadow.

Mabingwa watetezi Arsenal watakutana na Hull, marudio ya fainali ya 2014. Hii itakuwa mara ya tatu mfululizo kwa klabu hizo mbili kukutana katika dimba hilo. Gunners waliwabandua Hull kwenye raundi ya tatu mwaka jana baada ya kuwashinda 2-0.

Crystal Palace nao wakitembelea Tottenham na Bournemouth wacheze nyumbani dhidi ya Everton kwenye michezo itakayoshirikisha klabu za Ligi ya Premia pekee.

Mechi zitachezwa wikendi ya 19-22 Februari.

Meneja wa Chelsea Guus Hiddink amesema mechi kati ya klabu yake na Manchester City ndiyo “mechi kubwa” na itavutia sana mashabiki.

“Hiyo ni fainali tayari!” aliongeza.

Droo kamili:

  • Chelsea v Manchester City
  • Reading v West Brom or Peterborough
  • Watford v Leeds United
  • Shrewsbury Town v Manchester United
  • Blackburn v Liverpool or West Ham
  • Tottenham v Crystal Palace
  • Arsenal v Hull
  • Bournemouth v Everton