Falcao ashindwa kurejea Atletico Madrid

Falcao Haki miliki ya picha Getty
Image caption Falcao alifanikiwa sana alipokuwa Atletico Madrid

Mshambuliaji wa Chelsea Radamel Falcao alinyimwa nafasi ya kurejea Atletico Madrid siku ya mwisho ya kuhama kwa wachezaji.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia, ambaye yuko Chelsea kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Monaco, alikuwa Uhispania usiku wa Jumatatu akitumai angerejea kwenye klabu hiyo ya La Liga.

Lakini matumaini yake yalikatizwa pale Jackson Martinez, ambaye angeacha pengo Atletico, aliposhindwa kuhamia Uchina.

Hii ina maana kwamba hakukuwa na nafasi kwake kwenye klabu hiyo ya La Liga.

Falcao ameanza mechi moja pekee Ligi ya Premia akiwa Chelsea na bao pekee alilowafungia katika mechi 15 alizowachezea alilifunga baada ya kuingia kama nguvu mpya.

Falcao aumia tena Chelsea

Mchezaji huyo wa miaka 29 alitua Stamford Bridge Julai mwaka jana baada ya kushindwa kutamba akiwa Manchester United kwa mkopo msimu wa 2014-15.

Hajachezea Chelsea tangu tarehe 31 Oktoba.

Aliumia paja mapema mwezi Novemba na jeraha lake likazidi akicheza mechi ya mazoezi Desemba.

Katika miaka miwili aliyokuwa Atletico, Falcao alisaidia klabu yake kushinda Ligi ya Uropa 2012 na Kombe la Mfalme, maarufu kama Copa del rey, mwaka 2013.

Aliifungia klabu hiyo magoli 52 katika mechi 68.