Ushindi kwa Everton, sare kwa Chelsea

Chelsea Haki miliki ya picha Getty
Image caption Chelsea hawajashindwa tangu tarehe 14 Desemba

Chelsea wameendeleza rekodi yao ya kutoshindwa chini ya kaimu meneja Guus Hiddink hadi mechi saba katika Ligi ya Premia baada ya kutoka sare tasa na Watford.

Diego Costa alikaribia kufunga kipindi cha kwanza lakini mpira wake ukakosa goli pembamba, huku kombora la Etienne Capoue nalo likizimwa na kipa wa Chelsea Thibaut Courtois.

Heurelho Gomes alifanya kazi ya ziada kuzima mpira wa kichwa kutoka kwa Costa akitumia mkono mmoja na kuwanyima Chelsea ushindi dakika za mwisho mwisho.

Chelsea wamepanda alama moja hadi nambari 13 na alama 29, huku Watford wakiwa alama nne na nafasi nne juu ya Chelsea.

Kwingineko, Everton walipata ushindi wao wa kwanza ligini nyumbani tangu Novemba walipoandikisha ushindi dhidi ya Newcastle uwanjani Goodison Park.

Everton, ambao hawakuwa wameshinda mechi hata moja Ligi ya Premia tangu siku ya Boxing Day, walijiweka kifua mbele kupitia Aaron Lennon.

Ross Barkley Barkley baadaye alifunga mikwaju miwili ya penalti, ya pili ikitokana na madhambi ya Jamaal Lascelles ambaye alilishwa kadi nyekundu.

Vijana hao wa Roberto Martinez sasa wamepanda hadi nambari 11 ligini, huku Newcastle nao wakisalia nambari 18, alama mbili kutoka eneo la kushushwa daraja.