Valencia wabebeshwa magoli saba Barcelona

Suarez Haki miliki ya picha Getty
Image caption Luis Suarez alifunga magoli manne

Klabu ya Valencia chini ya nyota wa zamani wa Manchester United Gary Neville ilipokezwa kichapo cha mwaka na klabu ya Barcelona katika nusufainali ya michuano ya Copa del Rey baada ya kubebeshwa magoli saba.

Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza ilichezewa uwanjani Nou Camp.

Luis Suarez alifunga mabao manne, huku nyota wa Argentina Lionel Messi naye akijizolea magoli matatu.

Neymar alishindwa kufunga penalti.

Valencia walidhofishwa zaidi na hatua ya beki Shkodran Mustafi kumchezea visivyo Messi kipindi cha kwanza, kosa lililomfanya kufukuzwa uwanjani.

Neville hajashinda mechi hata moja ligini kati ya nane alizosimamia tangu kuchukua usukani Desemba.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Neville aliteuliwa kocha wa Valencia Desemba

Neville alikuwa amerejea uwanja ambao enzi yake ya uchezaji alipanda ushindi mkubwa na muhimu sana.

Akiwa na umri wa miaka 24, alikuwa kwenye timu ya United iliyoshinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kujikwamua dhidi ya Bayern Munich fainali ya 1999 uwanjani Nou Camp.

Akizungumza baada ya mechi hiyo dhidi ya Barca, Neville alisema siku hiyo ni moja ya siku zenye machungu zaidi katika maisha yake katika ulimwengu wa soka.