Voliboli: Kenya kukabiliana na Misri Yaounde

Kenya
Image caption Kenya ndio mabingwa wa Afrika

Timu ya taifa ya wanawake ya voliboli ya Kenya, ambao ndio mabingwa wa Afrika, itakutana na Misri kwenye nusufainali ya mashindano ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Rio mjini Yaounde leo.

Ukumbi wa Palais des sport mjini Yaounde huenda ukalipuka leo usiku mashabiki wakishangilia timu yao ya taifa, Cameroon, ikipambana na Algeria.

Timu hizo maarufu zitakuwa zinamenyana kwenye mechi za nusufainali za mashindano ya voliboli ya wanawake ya mataifa ya Afrika kugombania nafasi ya kushiriki michezo ya Olimpiki mwaka huu mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Algeria iliongoza kundi B ilipoishinda Misri kwa seti 3-1, Lydia Oulmou akiongoza wafungaji wa Algeria na pointi 10 naye Aya El Shami akawa mfungaji bora wa Misri na pointi 11.

Misri ilimaliza ya pili ikifuatwa na Botswana na ya mwisho Uganda ambayo iligeuzwa maembe na timu zote mpaka Botswana pia ikawashinda seti 3-2.

Kenya ilichukua nafasi ya kwanza kundi A baada ya kushinda Cameroon seti 3-1 Jumapili usiku, Lydia Maiyo akiongoza na pointi 15 naye mwenzake Joy Lusenaka akawa na pointi 15, huku Stephanie Fotoso akiwa mfungaji bora wa Cameroon na pointi 12.

Mbali na Maiyo na Lusenaka, miongoni mwa wachezaji wengine Kenya inategemea sana kwa ushindi ni nahodha Mercy Moim, Evelyn Makuto na dadake Violet Makuto, na Jane Wacu.