Aliyekabiliana na madawa katika riadha Urusi afariki

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Aliyekabiliana na madawa katika riadha Urusi afariki

Aliyekuwa mkuu wa shirika la kupambana na madawa ya kuongeza nguvu mwilini nchini Urusi ameaga dunia.

Nikita Kamaev ameaga dunia yapata miezi miwili pekee tangu ajiuzulu kufuatia ufichuzi wa shirikisho la riadha duniani kuhusu matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini miongoni mwa wanariadha nchini humo.

Shirikisho la riadha la Urusi RUSADA limesema kuwa Kamaev alikumbwa na mshtuko wa moyo.

Urusi ilipigwa marufuku kufuatia ufichuzi huo mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita.

Shirikisho linalopambana na madawa kututumua misuli duniani World Anti-Doping Agency (Wada) linailaumu serikali ya Urusi kwa kuendeleza sera ya siri inayoruhusu matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini.

''Marehemu atasalia katika kumbukumbu zetu kutokana na uadilifu wake na maono yake'' taarifa hiyo ya RUSADA ilieleza.

''Kamaev alilalamikia maumivu ya moyo baada ya kushiriki mchezo wa kuteleza kwenye barafu'' Alisema mkurugenzi wa zamani wa Rusada jenerali mstaafu Ramil Khabriev.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kifo chake kimetokea wakati ambapo Urusi imepigwa marufuku ya kutoshiriki mashindano yeyote ya riadha

Kifo chake kimetokea wakati ambapo Urusi imepigwa marufuku ya kutoshiriki mashindano yeyote ya riadha na kamati ya olimpiki duniani IOC na shirikisho la riadha duniani IAAF.

IAAF ilichukua hatua hiyo kali kufuatia ufichuzi huo.

Marufuku hiyo itaondolewa tu pale nchi hiyo itakapowashawishi wachunguzi wa kimataifa kuwa imevunja sera hiyo ya kuendeleza na kuficha matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini.

Urusi inajiunga na Argentina, Ukraine, Bolivia, Andorra na Israel kama mataifa yaliyothibitishwa kukiuka maadili dhidi ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini.

Kamaev alijiuzulu ilikuruhusu uongozi wa RUSADA kuweka mikakati mipya ya kuirejesha katika mashindano ya kimataifa ya riadha ikiwemo michezo ya Olimipiki ya yatakayoandaliwa Agosti mwaka huu huko Rio de Jenairo nchini Brazil.