Moyes: Van Gaal apewe muda zaidi Man Utd

Moyes Haki miliki ya picha PA
Image caption Moyes amesema Man Utd haifai kupata sifa za "klabu inayofuta mameneja"

Meneja wa zamani wa Manchester United David Moyes amesema klabu hiyo haifai kumfuta kazi Louis van Gaal licha ya klabu hiyo kuandikisha matokeo mabaya.

Kumekuwa na ripoti kwamba klabu hiyo imejiandaa kumfuta meneja huyo na kumpa kazi Mreno aliyefutwa kazi Chelsea mwezi Desemba Jose Mourinho.

Moyes, aliyefutwa kazi na klabu hiyo baada ya kufanya kazi miezi kumi pekee, amesema klabu hiyo haifai kupata sifa za “klabu inayofuta mameneja kiholela”.

Amesema ingawa klabu hiyo ilishindwa na klabu ya Midtjylland FC ya Denmark katika mechi ya Europa Leauge Alhamisi, bado kuna mechi ya marudiano nyumbani ambayo wanaweza kushinda.

Moyes mesema alisikitika sana alipofutwa kazi baada ya kufanya kazi miezi kumi pekee.

Lakini nyota wa zamani wa Newcastle United Alan Shearer amesema ni kama klabu hiyo haina matumaini hasa baada ya kushindwa 2-1 na Sunderland katika Ligi ya Premia.

Ameambia BBC Sport kwamba baada ya mechi hiyo, Van Gaal alionekana kama mtu aliyeishiwa na mawazo na aliyesalimu amri.

Kwa mujibu wa Shearer, uchezaji wao Europa League siku ya Alhamisi ulikuwa duni sana.

Baada ya kufutwa kazi Manchester, Moyes alipata kazi Real Sociedad nchini Uhispania lakini akafutwa kazi baada ya kukaa mwezi mmoja.