TP Mazembe washinda Super Cup

Mazembe Haki miliki ya picha Getty
Image caption TP Mazembe ndio mabingwa wa Afrika mwaka 2015

Klabu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeshinda kombe la Super Cup kwa mara ya tatu kwa kulaza Etoile du Sahel ya Tunisia.

Mazembe walipata ushindi wa 2-1 kwenye mechi hiyo iliyochezewa mjini Lubumbashi Jumamosi.

Mabingwa wa Afrika Mazembe pia walishinda kombe hilo linalokutanisha mshindi wa Ligi ya Klabu Bingwa barani Afrika na mshindi wa Kombe la Mashirikisho mwaka 2010 na 2011.

Etoile, walioshinda Kombe la Mashirikisho 2015, pia wameshinda Super Cup mara mbili.

Mazembe walishinda kupitia mabao mawili kutoka kwa mshambuliaji kutoka Ghana Daniel Nii Adjei mwenye umri wa miaka 27.

Adjei alifunga la kwanza dakika ya 20 na la pili dakika ya 45.

Sahel waliomboa bao moja dakika za mwisho kupitia Mohamed Msekni.