Mourinho hajahakiki kazi Manchester United

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jose Mourinho amesema kuwa hana uhakikika wa kuwa meneja wa Manchester United.

Aliyekuwa kocha wa Chelsea Jose Mourinho amesema kuwa hana uhakikika wa kuwa meneja wa Manchester United.

Mreno huyo hata hivyo anasema kuwa anamatumaini ya kurejea uwanjani msimu wa joto.

Taarifa hiyo inajiri takriban mwezi mmoja tangu BBC itangaze kuwa kocha huyo mbishi amefanya mazungumzo na wakala wa Manchester United.

Mourinho, 53, alifutwa kazi na mabingwa wa ligi kuu ya Uingereza Chelsea mwezi Desemba, takriban miezi 7 pekee baada ya kuinyakua kombe la ligi kuu ya Uingereza.

Alipoulizwa na wanahabari iwapo alikuwa njiani kumrithi Louis van Gaal uwanjani Old Trafford,

Mourinho alijibu : "Kwa hakika hilo ndilo swali kuu .''

Mourinho ambaye yuko Singapore, alisema :

"hakuna ajuaye iwapo yale tunayoyasoma magazetini ni ya ukweli au la, hata mimi mwenyewe sijui''

Mbali na Manchester United, Mourinho pia amehusishwa na klabu ya Serie A ya Italia Inter Milan mbali na mabingwa wa ligi kuu ya Uhispania Real Madrid.

"hata hivyo kuanzia msimu ujao nitakuwa na klabu kipya kwa mapenzi ya mungu.''

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mourinho hajahakiki kazi Manchester United

Hatma ya mholanzi Van Gaal, 64, imekumbwa na ati ati kufuatia msururu wa matokeo ya kutoridhisha.

kandarasi yake na mashetani wekundu inakamilika mwisho wa msimu ujao.

United wanashikilia nafasi ya 5 katika jedwali la ligi kuu ya Uingereza wakiwa ana alama 6 nyuma ya timu inayoorodheshwa ya nne Manchester City.

Timu nne za kwanza ndizo zinazofuzu kwa kombe la mabingwa barani Ulaya mwaka ujao.

Vilevile wamefuzu kwa robo fainali ya kombe la FA mbali na kuwa na tarehe dhidi ya FC Midtjylland katika mchuano wa timu 32 za kuwania kombe la Europa.

United ililazwa 2-1 FC Midtjylland katika mkondo wa kwanza.