Blatter, Platini wapunguziwa adhabu

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Joseph Blatter

Rais wa Shirikisho la kimataifa la Soka (FIFA) anayemaliza muda wake Joseph Blatter na Rais wa UEFA Michel Platini wamepunguziwa adhabu kutoka miaka 8 hadi 6,Uamuzi huu umetangazwa Jumatano hii na Shirikisho la kimataifa la Soka (FIFA), baada ya wawili hao kukata rufaa.

Hayo yanajiri wakati wagombea wawili kwenye nafasi ya urais wa FIFA, wakiwa na matumaini kwamba wataibuka washindi.

Kamati ya rufaa ya FIFA haikutoa uamzi mzuri kwa Blatter na Platini wanaoadhibiwa kwa sababu ya malipo yenye utata wa Euro milioni 1.8, zilizotolewa na Blatter akimlipa Platini mwaka 2011 kwa ajili ya kazi ya kushauriana iliyomalizika tangu mwaka 2002.

Kamati hiyo imebaini kwamba wawili hawa wamekutwa na hatia ya kukiuka Ibara nne za maadili ya sheria na wamekutwa hasa na hatia ya mgogoro wa kimaslahi.

Wakati huo huo, Tume hiyo imefutilia mbali madai ya "rushwa" na kufuta rufaa ya kitengo cha uchunguzi cha FIFA ambacho kiliomba Joseph Blatter na Michel Platini wasimamishwe maisha katika shughuli zote zinazohusiana na soka.

Kwa sasa wawili hawa hawana tena matumani ya kufutiwa makosa yanayowakabili, kazi kubwa imebaki kwa Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (TAS), ambayo ni Mahakama ya ngazi ya juu katika michezo.

Uamuzi huo mpya wa FIFA ni pigo kubwa kwa Michel Platini, ambae tayari amelazimishwa kuachana kuwania katika kinyan'ganiro cha urais wa FIFA, ambapo alikua amepewa nafasi kubwa ya kumrithi Joseph Blatter.