Manchester United kumkosa De Gea tena

De Gea Haki miliki ya picha EPA
Image caption De Gea aliumia akijiandaa kwa mechi dhidi ya FC Midtjylland nchini Denmark

Klabu ya Manchester United itakuwa bila kipa David de Gea kwa mechi ya tatu mfululizo itakapowakaribisha nyumbani vijana wa FC Midtjylland kutoka Denmark mechi ya Europa League leo jioni.

De Gea hajacheza mechi mbili tangu aumie goti akipasha misuli moto kabla ya mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya FC Midtjylland wiki iliyopita nchini Denmark.

United walilazwa 2-1.

“Hatacheza, hilo nina uhakika nalo,” amesema meneja wa Manchester United Louis van Gaal.

Winga Antonio Valencia anakaribia kuwa sawa kucheza lakini hataweza kucheza leo pia.

Valencia hajacheza tangu afanyiwe upasuaji mguuni Oktoba.

Beki Chris Smalling atachunguzwa baada ya kugonga ubao wa matangazo wakati wa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Shrewsbury Jumatatu, mechi ambayo United walishinda.

Donald Love huenda akachezeshwa tena huku naye Marcos Rojo akitarajiwa kuchezeshwa dakika 20.

Mshambuliaji Wayne Rooney, kiungo wa kati Marouane Fellaini na beki Matteo Darmian bado wanauguza majeraha.

Van Gaal amesema United watakuwa “wabunifu sana” kujaribu kulipa deni la mechi ya mkondo wa kwanza na kuondoka na ushindi.

“Lazima tufunge, hilo ni wazi. Lazima tuwapangue na kwa hivyo itabidi tuwe wajanja sana,” ameongeza.