Pellegrini: Ilikuwa busara kuangazia Ulaya

City Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Man City walichapwa 5-1 Kombe la FA

Meneja wa Machester city Manuel Pellegrini amesema uamuzi wake wa kuangazia zaidi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya badala ya Kombe la FA ulizaa matunda baada ya ushindi walioupata dhidi ya Dynamo Kiev Jumatano.

Pellegrini alishtumiwa kwa kuichezesha timu hafifu siku ya Jumapili ambapo walichapwa mabao 5-1 katika mechi ya raundi ya tano ya FA mikononi mwa Chelsea.

Lakini Jumatano, walishinda mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mabao 3-1.

“Nilikuwa na wachezaji 13 pekee wa kikosi cha kwanza waliokuwa sawa kucheza, ulikuwa uamuzi wa busara kuwapumzisha mechi hiyo ya FA,” alisema Pellegrini.

“Ilikuwa muhimu kwa sababu ilitubidi kucheza mechi hii (ya Ulaya) kwa ukali.”

Pellegrini alifanya mabadiliko mara 10 kwenye kikosi kilichocheza kombe la FA na kuweka kikosi imara mechi hiyo ya Kiev.

Sergio Aguero, David Silva na Yaya Toure walifungia City, naye Mlinda lango wa Uingereza Joe Hart, ambaye pia hakuchezeshwa mechi hiyo ya Kombe la FA akiokoa mpira muhimu kutoka kwa Vitaliy Buyalsky.

Pellegrini aliongezea: “Katika taaluma hii kila mara unapata malalamiko iwapo hutashinda , lakini kwa mameneja ni muhimu kufanya uamuzi bora.”

“Mimi hujaribu kuheshimu mashindano yote lakini kwa bahati mbaya hatutaweza kuendelea na Kombe la FA.”