Wachezaji wa Nigeria watuzwa miaka 30 baadaye

Jonathan Akpoborie Haki miliki ya picha
Image caption Jonathan Akpoborie, mmoja wa wachezaji hao, baadaye alichezea timu kuu ya taifa mara 13

Kikosi cha Nigeria kilichoshinda ubingwa wa dunia kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 16 kipetuzwa baada ya kusubiri miaka 30.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametimiza ahadi yake ya kuwatuza aliyoitoa alipokuwa kiongozi wa kijeshi wakati wa michuano hiyo ya 1985.

Nduka Ugbade, nahodha wa timu hiyo iliyolaza Ujerumani Magharibi kwenye fainali mjini Beijing ameambia BBC Sport kuwa: “Nimepokea pesa zangu, hatimaye.”

“Nimefurahi sana kwamba rais wetu ametimiza ahadi yake.”

Buhari alikuwa amewaahidi wachezaji hao nyumba, hisa katika benki kuu na ufadhili wa kimasomo miongoni mwa zawadi nyingine. Lakini serikali yake ilipinduliwa na hakuweza kutimiza ahadi yake.

Buhari, aliyechaguliwa kuwa rais mwaka jana, alitangaza Januari mwaka huu kwamba atatoa zawadi ya naira milioni mbili ($10,000; £7,000) kwa kila mchezaji na 1.5m kwa maafisa wa timu.

"Yeye ni mtu wa kutimiza ahadi na kwa niaba yangu binafsi na timu namshukuru sana rais,” ameongeza Ugbade.

Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Kingsley Aikhionbare, alifariki akiwa London mwaka 1996. Baada ya wachezaji kupewa pesa zao, walikaa kimya dakika moja kumkumbuka.

Mashindano yao ya ubingwa wa dunia wa wachezaji wa chini ya miaka 16 yaliandaliwa mara tatu kabla ya kubadilishwa na kuwa Kombe la Dunia kwa wachezaji wa chini ya miaka 17 mwaka 1991.

Nigeria walishinda Kombe la Dunia la wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17 mnamo 1993, 2007, 2013 na 2015.