Arsenal kumkosa Cech wakikabili Spurs

Cech Haki miliki ya picha Getty
Image caption Cech aliumia wakati wa mechi dhidi ya Swansea

Arsenal watamkosa mlinda lango wao Petr Cech mechi kali dhidi ya mahasimu wao wa London Tottenham Hotspur uwanjani White Hart Lane Jumamosi.

Kipa huyo anauguza jeraha la mtoki.

Cech aliumia dakika za mwishomwisho za mechi ambayo walilazwa 2-1 nyumbani na Swansea City baada yake kuruka juu kufikia mpira wakati wa kona.

"Alikuwa anatatizwa kiasi na mtoki kabla ya mechi na nadhani amesumbuka kwenye mechi hii,” meneja wao Arsene Wenger alisema baada ya mechi hiyo.

Beki wao Laurent Koscielny pia hataweza kuwachezea debi hiyo ya London kutokana na jeraha mguuni.

Koscielny, 30, hakuwachezea mechi dhidi ya Swansea.

Haki miliki ya picha AFP

Cech, 33, aliyehamia Emirates kutoka Chelsea, amewachezea Gunners mechi 28 Ligi ya Premia.

Arsenal wataenda kwenye mechi hiyo wakiwa nafasi ya tatu kwenye jedwali, alama sita nyuma ya viongozi Leicester City, zikiwa zimesalia mechi 10 msimu huu.