Shabiki wa Leicester City aridhika na £72,000

Leicester Haki miliki ya picha Getty
Image caption Leicester wameshangaza wengi msimu huu kwa kukwamilia kileleni

Shabiki wa Leicester City ambaye alikuwa na nafasi ya kushinda £250,000 iwapo klabu hiyo ingeshinda Ligi ya Premia msimu huu ameamua kuuza dau yake mapema.

Shabiki huyo, aliyeweka dau ya £50, ameuza dau yake £72,000.

Mwanamume huyo kutoka Warwickshire, ambaye hakutaka kufichua jina lake, alijiondoa Jumamosi.

Iwapo angekuwa na subira, saa chache baadaye dau yake ingekuwa na thamani ya £91,000 baada ya Leicester kulaza Watford 1-0.

Shabiki huyo hata hivyo hana majuto na alisema: "Itakuwa na maana kubwa sana kwangu tukishinda ligi, kwa hivyo hakuna haja ya kuwa na tamaa.”

Amesema atafuatilia kwa karibu mechi zilizosalia.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mahrez na Wardy wameisaidia sana Leicester

"Mambo yanabadilika sana. Hata Chelsea wanaweza wakarejea katika nne bora siku za mwisho mwisho,” akasema.

Anapanga kulipa mkopo wa nyumba akitumia pesa hizo kisa zilizosalia azitumie kwenda likizoni Uhispania.