Mambo matano muhimu kumhusu Maria Sharapova

Sharapova Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sharapova ameshinda mataji matano ya Grand Slam

Bingwa wa zamani wa mchezo wa tenisi duniani Maria Sharapova amekiri kwamba alipatikana akiwa ametumia dawa zilizoharamishwa wakati wa mashindano ya Australian Open. Haya hapa ni mambo matano ufaayo kuyajua kuhusu nyota huyu wa tenisi.

Haki miliki ya picha Getty

1. Alianza kucheza tenisi ya kulipwa akiwa na miaka 14

Bi Sharapova alianza kucheza tenisi akiwa na umri mdogo sana na akiwa na umri wa miaka minane alishiriki mashindano ya kirafiki yaliyomhusisha bingwa wa tenisi Martina Navratilova mjini Moscow.

Alikuwa na umri wa miaka tisa alipowasili katika Akademi ya Tenisi ya Nick Bollettieri jimbo la Florida, akiwa na babake Yuri.

Haki miliki ya picha Getty

Mamake, Yelena, alisalia Siberia na hakuonana na wawili hao kwa miaka miwili iliyofuata kutokana na matatizo ya viza.

Bw Bollettieri mara moja alitambua kipaji cha msichana huyo na akiwa na umri wa miaka 14 akaanza kucheza tenisi ya kulipwa.

2. Alijizolea $29.5m (£21m) mwaka 2015 pekee

Mwanatenisi huyu mwenye umri wa miaka 28 amekuwa miongoni mwa wachezaji wa kike waliolipwa pesa nyingi sana duniani kwa miaka 11 iliyopita, kwa mujibu wa Forbes.

Haki miliki ya picha Getty

Mwaka 2015 alipata jumla ya $29.5m kutoka kwa tenisi pekee kwa mujibu wa Forbes. Ana pia mikataba naEvian, Tag Heuer, Porsche, Avon na Nike.

Baada ya kukiri kutumia dawa zilizoharamishwa, Nike, walioingia mkataba naye miaka 11 iliyopita, wamesimamisha mkataba wao naye.

Kampuni ya Uswizi ya Tag Heuer pia imevunja uhusiano naye.

3. Ameshinda mataji matano ya Grand Slam

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Alishinda taji la kwanza la Grand Slam akiwa na miaka 17 mwaka 2004

Sharapova aliibuka kuwa mwanamke mchanga zaidi kutwaa ubingwa Wimbledon akiwa na umri wa miaka 17 mwaka 2004 na mwaka uliofuata aliorodheshwa nambari moja duniani.

Mwaka 2006, alishinda US Open, na pia akatwaa ubingwa Melbourne mwaka 2008.

Alitatizwa na jeraha na kufikia mwisho wa 2010 aliorodheshwa nambari 18 duniani.

Mwaka 2012, alianza kuvuma tena na akamshinda Sara Errani na kushinda French Open mjini Paris.

Mwaka huo pia alitwaa tena ubingwa wa dunia na kushinda fedha katika Olimpiki.

Alishinda taji la pili la French Open mwaka 2014.

4. Familia yake iliishi karibu na Chernobyl

Familia yake ilikuwa ikiishi maili 80 (kilomita 130) kaskazini mwa kiwanda cha nyuklia cha Chernobyl vinu vinne vilipolipuka 1986. Wazazi wake walitoroka Yelena alipokuwa na mimba ya Sharapova.

Haki miliki ya picha AFP

Walienda kuishi mji mdogo wa Nyagan, eneo la Siberia ambako harapova alizaliwa na kulelewa.

Ametoa pesa za kusaidia eneo la Gomel, Belarus lililoathiriwa na mkasa huo wa Chernobyl.

Aidha, alianzisha wakfu wa Maria Sharapova Foundation na huwa balozi mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo (UNDP).

5. Amepatikana ametumia dawa aina ya meldonium

Bingwa huyu wa zamani alitangaza tarehe 7 Machi kwamba alipatikana ametumia dawa aina ya meldonium, inayotumiwa na watu wanaougua angina, ambao ni ugonjwa unaomfanya mtu kuumwa na kifua na wakati mwingine bega, mikono na shingo.

Haki miliki ya picha Getty

"Nakubali lawama,” amesema Bi Sharapova.

Amesema amekuwa akitumia dawa hiyo ya meldonium "kwa miaka 10 " iliyopita baada ya kupewa na daktari wake kutibu masuala kadha ya kiafya.

Hata hivyo alisema alifahamu dawa hiyo kuwa mildronate na ni majuzi tu alipogundua kwamba jina lake jingine ni meldonium na kwamba ilikuwa hivi karibuni imeorodheshwa na Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Dawa katika Michezo (WADA) kwenye orodha ya dawa zilizopigwa marufuku.

Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) limesema hataruhusiwa kucheza kuanzia tarehe 12 Machi.

Haki miliki ya picha PA

“Nilifanya kosa kubwa,” amesema. “Nimewavunja moyo mashabiki wangu na mchezo huu ambao nimekuwa nikiucheza tangu nikiwa na miaka minne, na ninaoupenda sana.

"Najua kwamba kwa hili, nitaadhibiwa na sitaki kumaliza uchezaji wangu hivi. Natumai nitapewa fursa nyingine ya kuendelea kucheza mchezo huu.”