Mabondia wa Kenya na Ethiopia watamba

Image caption Nick Okoth wa Kenya

Bondia wa Kenya na Ethiopia wamefuzu kwa robo-fainali ya mashindano ya ndondi yanayoendelea Yaounde.

Bondia wa Uganda aliyeshinda mechi ya awali ameng'olewa mashindanoni.

Nick Okoth wa Kenya na Mesfin Keralah wa Ethiopia jana usiku walishinda mapigano yao uzani mwepesi katika mashindano ya Afrika ya kufuzu kwa michezo ya Olympiki yanayoendelea mjini Yaounde, mji mkuu wa Cameroon..

Lakini chombo kikamwendea mrama bondia wa Uganda Sulaiman Segawa aliyeshindwa na Reda Benbaziz wa Algeria uzani wa mwepesi.

Okoth naye alitolewa jasho na Mohlerepe Qhobosheane wa Lesotho kabla ya kuibuka mshindi wa pointi 2-1, huku Kerale wa Ethiopia akimshinda Paulo Britos wa Msumbiji..

Okoth sasa anakutana na Reda Benabaziz wa Algeria robo-fainali Jumatano ijayo na Kerale anazipiga na Andrik Allisop wa Ushelisheli.

Bondia mwingine wa Kenya ambaye yuko robo-fainali ni Rayton Okwiri ambaye alifuzu moja kwa moja baada ya droo kufanyika..

Okwiri atakutana na Christian Abua wa Nigeria ama Adamou Kohautto kwenye robo fainali..

Katika uzani mzito matumaini ya Kenya na Uganda kusonga mbele yalizimwa na mabondia kutoka Misri na Nigeria.

Fredrick Ramogi wa Kenya alishindwa kwa wingi wa pointi na Mostafa Hafez wa Misri naye Michael Dekabembe akaondolewa kwa pointi na Efe Ajagba wa Nigeria.

Leo hii Simon Mulinge uzani wa 'fly', Benson Gicharu uzani wa bantam, wote wa Kenyua na Atamas Mugerwa wa Uganda uzani wa bantam watapanda ulingoni.

Mulinge anapigana na Muyideen Oyakojo wa Nigeria, Gicharu anazipiga dhidi ya Emmanuel Ngoma wa Zambia na Mugerwa ana mlima wa kupanda dhidi ya Hesham Mahmoud wa Misri.

Mabondia wengine wa Kenya ambao wana mapigano leo hii ni Elly Ajowi na kwa upande wa wanawake ni Christine Ongare na Teresia Wanjiru...

Ajowi, mshindi wa shaba katika michezo ya mataifa ya Afrika mwaka jana, anapambana na Christian Tsoye wa Cameroon uzani wa mzito.

Ongare naye anakutana na Lewissia Nzamba Nzamba wa Gabon uzani wa 'fly' huku Wanjiru akilimana na Hasnaa Lachgar wa Morocco..