Antonio Conte kuondoka Italy- Tavecchio

Rais wa Shirikisho la Soka la Italia amethibitisha kuwa Antonio Conte ataacha kuinoa Italia baada ya michuano ya Euro 2016.

Inadaiwa kuwa meneja huyo wa zamani wa Juventus anataka kuchukua kibarua cha kuinoa Chelsea mwanzoni mwa msimu ujao baada ya kufanya vikao kadhaa kujadili suala hilo.

Akihojiwa rais huyo wa FIGC, Carlo Tavecchio amesema Conte anatarajia kuondoka baada ya michuano hiyo ya Ulaya hivyo kutoa mwanya kwa Chelsea kuongeza juhudi za kumnasa.

Chelsea imekuwa katika mawindo ya kutafuta meneja mpya wa kudumu ambaye atachukua nafasi ya Jose Mourinho aliyetimuliwa Desemba mwaka jana.

Guus Hiddink amekuwa meneja wa muda wa Chelsea toka Mourinho aondoke Stamford Bridge na anatarajiwa kuondoka baada ya kumalizika kwa msimu huu.