Arsenal kushuka dimbani Barcelona

Arsenal Haki miliki ya picha Arsenal Barcelona
Image caption Arsenal walilazwa 2-0 mechi ya kwanza uwanjani Emirates

Klabu ya Arsenal ya Uingereza itashuka ugani Nou Camp kwa mechi ya marudiano dhidi ya miamba wa Ulaya Barcelona, wakikabiliwa na kibarua kigumu katika juhudi za kutaka kufika robofainali.

The Gunners wako nyuma 2-0 baada ya kushindwa mechi ya mkondo wa kwanza nyumbani Emirates.

Meneja wao Arsene Wenger amesema wachezaji wake wamejiandaa kucheza vyema na kwamba ni muhimu sana kwao kufunga.

“Hatuhitajiki kufanya hesabu sana, tunajua ni lazima tushambulie na tufunge,” amesema Wenger.

“Wachezaji wameungana pamoja tayari kucheza vyema.”

Arsenal wanahitaji kufunga mabao mawili Nou Camp bila kufungwa bao jingine ndipo angalau wajipe matumaini ya kusonga.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wenger ansema Arsenal watahitaji kushambulia sana

Walikuwa wamejikakamua sana mechi ya mkondo wa kwanza lakini wakaumbuliwa na mabao mawili ya Lionel Messi dakika 20 za mwisho.

Beki wa Arsenal Laurent Koscielny atarejea kuwaongeza nguvu baada ya kukaa nje kutokana na jeraha.

"Tumeshinda katika kila uwanja Ulaya lakini huko (Nou Camp) hatujafanikiwa bado,” anasema Wenger.

"Mtazamo wetu haukuwa mbaya lakini tuliteleza na tukaadhibiwa.

"Itatupa moyo sana kipindi kilichosalia cha msimu iwapo tutacheza vyema Jumatano.

"Huwa twapigana kushinda vikombe na kwa sasa hatupigiwi upatu kushinda msimu huu. Lakini bila kujali changamoto, Ligi ya Premia bado iko wazi na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya nafasi ni finyu sana.”

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Messi ndiye aliyefungia Barca mabao mechi ya kwanza

Barcelona, chini ya mkufunzi wao Luis Enrique, wamo alama nane mbele La Liga na wanapigania kuwa klabu ya kwanza kuhifadhi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya tangu kubadilishwa jina kutoka Kombe la Ulaya 1992.

Mechi itaanza saa 22:45 saa za Afrika Mashariki.

Mechi nyingine ya hatua ya 16 bora inayochezwa leo ni kati ya Juventus na Bayern Munich.