Leicester City wazidi kutisha Uingereza

Mahrez
Image caption Mahrez alifungia Leicester bao dakika ya 34

Leicester City wamefungua mwanya wa alama nane kileleni mwa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kuwalaza Crystal Palace kupitia bao la Riyad Mahrez Jumamosi.

Kwa sasa wana alama 66 baada ya kucheza mechi 31, klabu ya pili ikiwa Tottenham na alama 58 baada ya kucheza mechi 30.

Mahrez alipoteza nafasi wazi baada ya kupewa pasi safi mapema kwenye mechi lakini alifidia baada ya kurushiwa krosi na Jamie Vardy dakika ya 34 na akafunga.

Damien Delaney aligonga mwamba wa goli upande wa Crystal Palace dakika za mwisho mwisho lakini Leicester City walikwamilia uongozi wao na wakaondoka na ushindi.

Palace wamefika nusufainali Kombe la FA lakini hawajashinda mechi yoyote ligini tangu tarehe 19 Desemba.

Meneja wa Leicester Claudio Ranieri sasa ameongeza kadirio lake la kushinda ligi msimu huu kutoka alama 79 hadi alama 82 ambazo ndizo alama za juu zaidi ambazo Tottenham wanaweza kufikia iwapo watashinda mechi zao zote zilizosalia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mahrez na meneja Claudio Ranieri

Leicester watatwaa ubingwa wakishinda mechi sita kati ya saba walizosalia nazo na kufikia alama 84, hata kama Spurs au timu nyingine zinazopigania taji zitashinda mechi zote zilizosalia.

Vijana hao wa Ranieri sasa wameshinda mechi 13 kwa bao moja pekee msimu huu, idadi ya juu kushinda klabu nyingine zote ligi kuu.

Aidha, wana rekodi bora zaidi ugenini wakiwa wameshinda mechi 10 zao ugenini.

Leicester watapiga hatua zaidi kukaribia taji lao la kwanza kabisa ligini watakapokuwa wenyeji wa Southampton tarehe 3 Aprili.

Palace watajaribu kufikisha kikomo rekodi yao ya kutoshinda mechi 13 mfululizo watakapokuwa wageni wa West Ham tarehe 2 Aprili.