CAF: Rwanda 5-0 Mauritius -Matokeo

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rwanda 5-0 Mauritius

Amavubi Stars ya Rwanda imeweka bayana ari yake ya kufuzu kwa dimba la mataifa ya Afrika itakayoandaliwa mwakani huko Gabon.

Rwanda iliinyeshea Mauritius mabao 5-0 kwa nunge katika mechi ya marudio iliyochezewa mjini Kigali leo jioni.

Ernest Sugira alifunga mabao mawili ya haraka na kuwaweka wenyeji hao kifua mbele katika mechi hiyo ya kundi H.

Vijana hao wa kocha Johnny McKinstry hawakutosheka na hayo ,Dominique Nshuti alihakikisha timu yake imekwenda mapumzikoni ikiongoza kwa mabao 3-0.

Baada ya mapumziko Fitina Omborenga na Jean-Baptiste Mugiraneza walifuta machungu ya kichapo cha 1-0 walichopata katika mkondo wa kwanza siku tatu tu zilizopita.

Image caption Ethiopia 3-3 Algeria

Kufuatia ushindi huo Rwanda imeimarika hadi nafasi ya pili katika kundi lake wakiwa na alama 6, nne nyuma ya Black Stars ya Ghana.

Katika matokeo mengine, Ethiopia ilitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Desert Foxes ya Algeria mjini addis Ababa.

Algeria ambao wanaongoza kundi lao walilazimika kufanya kazi ya ziada baada ya wenyeji wao kuongoza mara mbili.

Algeria waliichapa Ethiopia, 7-1 mjini Blida timu hizo zilipokutana Ijumaa iliyopita katika mkondo wa kwanza.

Licha ya matokeo hayo Algeria wanaongoza kundi J na alama 10 5 zaidi ya Ethiopia.

Image caption Malawi 1-2 Guinea

Kila mshindi katika makundi yote 13 atajikatia tikiti ya moja kwa moja kucheza Gabon.

Hata hivyo timu mbili zilizomaliza na alama nyingi katika nafasi ya pili pia zitajiunga na mwenyeji katika kindumbwendumbwe hicho.

Huu hapa mukhtasari wa matokeo ya mechi zilizochezwa leo.

#AFCON2017

Rwanda 5-0 Mauritius

Namibia 1- 3 Burundi

Malawi 1-2 Guinea

Togo 0-0 Tunisia

Angola 0-2 DR Congo

Liberia 2-0 Djibouti

Uganda 0-0 Burkina Faso

Ethiopia 3-3 Algeria

Niger 1-2 Senegal

Namibia 1-0 Burundi

Togo 0-0 Tunisia

Lesotho 1-0 Seychelles.