Conte ateuliwa meneja wa Chelsea

Conte Haki miliki ya picha AP
Image caption Conte kwa sasa ni meneja wa timu ya taifa ya Italia

Meneja wa timu ya taifa ya Italia Antonio Conte ameteuliwa kuwa meneja mpya wa klabu ya Chelsea ya Uingereza, kwanzia mwisho wa msimu huu.

Mkufunzi huyo wa zamani wa Juventus mwenye umri wa miaka 46 ataanza kutumikia mkataba wake wa miaka mitatu baada ya kuongoza Italia michuano ya Euro 2016.

"Ninajivunia kuwa kocha wa timu ya taifa langu na ni wadhifa wa kuvutia sana kama kuwa meneja wa Chelsea ambao unaweza kufuata,” amesema.

Guus Hiddink, aliyechukua majukumu baada ya Jose Mourinho kufutwa, ataendelea kunoa Blues hadi mwisho wa msimu.

Fainali za Euro 2016 zitachezwa 10 Julai.

Conte atakuwa Mwitaliano wa tano kuwa meneja wa Chelsea baada ya Gianluca Vialli, Claudio Ranieri, Carlo Ancelotti na Roberto di Matteo.