Kichuya mchezaji bora wa Machi

Image caption Shiza Ramadhani Kichuya

Mshambuliaji Shiza Ramadhan Kichuya wa timu ya Mtibwa Sugar amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Machi kwa Ligi Kuu Tanzania Kichuya alionyesha kiwango cha juu katika mwezi huo uliokuwa na raundi nne, hivyo kuisaidia timu yake kushinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza.

Katika mechi hizo ambazo zote Kichuya alicheza, alifanikiwa kufunga mabao mawili kati ya matano yaliyofungwa na timu yake. Alifunga dhidi ya Coastal Union kwa ushindi wa mabao 3-0, na JKT Ruvu Stars ambapo Mtibwa Sugar ilishinda mabao 2-1.

Washindani wa karibu wa Kichuya walikuwa washambuliaji Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar, na Abdulrahman Mussa wa JKT Ruvu Stars ambao pia waling'ara kwa upande wa timu zao kwa mwezi huo.

Kichuya ambaye huu ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu, kwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora kwa Machi atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo.