Afrika K. Michezo isiyo na weusi ni marufuku

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Waziri wa michezo Fikile Mbalula

Afrika Kusini haitaandaa mashindano ya Raga, Kriketi, Riadha na Netiboli baada ya serikali kupiga marufuku shirikisho hizo nne kwa kukikuka kanuni zinazopendekeza kuwepo kwa wachezaji weusi katika timu za taifa.

Waziri wa michezo Fikile Mbalula amesema kuwa raga, kiriketi, riadha na netiboli itaathiriwa na marufuku hiyo.

Waziri Mbalula alisema kuwa serikali haitaruhusu kamwe uwenyeji wa mashindano hayo manne kwa sababu yameshindwa ketekeleza matakwa yao kikatiba kuongeza idadi ya wachezaji weusi katika timu za taifa.

Kauli hiyo ni pigo kubwa kwa shirikisho la raga la Afrika Kusini kwani ilikuwa imepanga kuwania uwenyeji wa mashindano ya dunia ya mwaka wa 2023.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Afrika Kusini yapiga marufuku michezo minne

Mwandishi wa BBC nchini humo anasema kuwa zaidi ya miongo miwili tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu nchini Afrika Kusini, mashirika ya michezo nchini humo mara nyingi hulaumiwa kwa kuwa na wazungu wengi kuliko wachezaji waeusi.

Aidha Mbalula amekuwa akiishawishi shirikisho hilo la raga kuwakuza wachezaji weusi bila mafanikio.

Mashirikisho hayo makubwa ya michezo nchini humo yalitia sahihi mkataba wa kuimarisha idadi ya wachezaji weusi mwaka wa 2014 hata hivyo kufikia sasa ni shirikisho la kandanda pekee lililotimiza matakwa hayo.

Hii inamaanisha kuwa mashirikisho hayo manne hayataruhusiwa kuandaa ama hata kuwania uwenyeji wa mashindano yeyote ya kimataifa.

Kamati maalum itakutana mwishoni mwa mwaka wa 2018 kutathmini maendelea ya mashirikisho hayo manne.

Marufuku hiyo hata hivyo haitaathiri uwenyeji wa michezo ya jumuiya ya madola ya mwaka wa 2022 ambayo imeratibiwa kufanyika mjini Durban Afrika Kusini.