Tiger Woods ajiandikisha kushiriki US Open

Woods Haki miliki ya picha PA
Image caption Woods hajashiriki mashindano tangu Agosti mwaka jana

Mchezaji nyota wa mchezo wa gofu Tiger Woods amejisajili kucheza mashindano ya US Open, ishara kwamba anajiandaa kurejea uwanjani.

Bingwa huyo mara 14 duniani amefanyiwa upasuaji mara tatu mgongoni na mara yake ya mwisho kucheza katika michuano yoyote ilikuwa Agosti 2015.

Hali ya kipekee ya Woods katika mashindano ina maana kwamba yuko huru kujitokeza na kucheza akitaka, lakini kujisajili kwake pia si thibitisho kwamba atashiriki michuano hiyo ya Oakmont tarehe 16 Juni.

Wakala wake Mark Steinberg ameambia ESPN kwamba hatua hiyo ni “utaratibu tu”.

Woods pia alijiandakisha kushiriki mashindano ya mwaka jana ya US Open lakini akajitoa baadaye kutokana na matatizo ya mgongo.

Mapema mwezi huu, Woods alisema hangeshiriki mashindano ya Masters yaliyoandaliwa Augusta.

“Nimekuwa nikigonga mipira na kufanya mazoezi kila siku, lakini mwili wangu hauko tayari,” alisema wakati huo.