Timu ya raga ya Kenya kulenga ubingwa Paris

Kenya
Image caption Kenya ilishindwa ubingwa mara ya kwanza katika Singapore Sevens

Timu ya raga ya Kenya ya wachezaji saba iliyoshinda taji la Singapore Sevens inalenga kuandikisha matokeo bora katika mashindano ya raga duniani ambayo yataandaliwa Ufaransa kuanzia tarehe 13 mwezi Mei mjini Paris, Ufaransa.

Ikiwa imesalia mizunguko miwili kabla ya msururu wa mechi hizo kukamilika nchini Uingereza, timu hiyo maarufu kama Shujaa inasaka kujiimarisha kabla ya kuingia uwanjani dhidi ya Ureno.

Kenya iko katika kundi 'A' pamoja na New Zealand,Urusi na Ureno.

Nahodha wa timu hiyo Andrew Amonde ameiambia BBC kuwa ubingwa wao mjini Singapore, umewamotisha kufanya vyema na watajitahidi kukusanya alama zaidi kwenye michuano ya Paris.

''Macho yetu yako Paris, na tuna matumaini kufanya vyema,'' alieleza.

Katika mashindano ya Singapore, Kenya ilikusanya alama 22 ikilinganishwa na mechi zake za awali ambapo haikuweza kufikisha alama 20.

Collins Injera anayekimbiza kuvunja rekodi ya mchezaji wa zamani wa Argentina Santiago Gomez Cora, aliye na 'trai' 230, ameeleza kuwa ingawa jedwali lao ni ngumu, watatia bidii kurudi na kikombe.

''Ni ukweli tuna wapinzani wazoefu, kama New Zealand lakini lengo letu ni kuandikisha matokeo mazuri,'' alisema Injera.

Image caption Wachezaji hao walikaribishwa ikulu na Rais Kenyatta

Shujaa wanashikilia nafasi ya saba katika jedwali hilo wakiwa na alama 85.

Kenya iliizaba Fiji 30-7 wiki chache iliyopita, na kuondoka na taji hilo.

Timu hiyo ilialikwa katika ikulu ya taifa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kufanya vyema Sinagpore.