Nigeria yatumai Mikel atacheza A. Kusini

John Obi Mikel
Image caption Kiungo cha Chelsea na timu ya taifa ya Nigeria.

Shirikisho la soka la Nigeria limesema kuwa kiungo wa nchi hiyo, John Obi Mikel, atakuwa amepona majeraha kabla ya mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Colombia mjini London, tarehe 30 Mei, kujiandaa kwa kombe la dunia.

Kulikuwa na wasi wasi kuwa baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 kuumia kwenye mechi dhidi ya Tottenham siku ya Jumamosi.

"Bahati nzuri majeraha hayatakwamisha fursa yake ya kucheza kombe la dunia kama ilivyohofiwa awali," msemaji wa NFF, Ademola Olajire aliieleza BBC.

"Ataweza kushiriki vyema katika mazozi," aliongeza.

"Mikel na Chelsea wamethibitisha kuwa alijeruhiwa, lakini ataweza kupata nafuu haraka kuliko ilivyodhaniwa."

Hata hivyo hataweza kucheza mechi zilizosalia za Chelsea katika ligi kuu ya soka ya England, ambapo timu hiyo inawania vikombe viwili ikiwa ni pamoja na FA.

Wakati huo huo, NFF imeeleza kuwa mechi pekee ya kirafiki iliyothibitishwa kwa Super Eagles kabla ya kombe la dunia, itakuwa ni kucheza na Colombia, mwezi Mei mjini London.