Blatter kupatanisha CAF na Togo

Wachezaji wa timu ya taifa ya Togo baada ya kushambuliwa.
Image caption Wachezaji wa timu ya taifa ya Togo baada ya kushambuliwa.

Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA, Sepp Blatter atakuwa mpatanishi katika mgogoro kati ya Togo na shirikisho la soka barani Afrika, CAF.

CAF iliipiga Togo marufuku ya kushiriki katika mashindano yake yote kwa muda wa miaka minne.

Uamuzi huo uliafikiwa baada ya Togo kujiondoa kwenye fainali za mashindano hayo yaliofanyika nchini Angola baada ya maafisa wake wawili kuuwawa wakati basi lao liliposhambuliwa kwa risasi katika eneo la Cabinda.

CAF ilidai serikali ya Togo iliingilia kati masuala ya usimamizi wa soka kwa kuamuru, kikosi chake kujiondoa kwenye fainali hizo na kurejea nyumbani.

Lakini Togo imepinga hatua hiyo na kulishitaki shirikisho la CAF katika mahakama ya kimataifa ya upatanishi CAS iliyoko nchini Uswisi.

Sasa kesi hiyo imesimamishwa huku Bw Blatter akijitayarisha kufanya kikao cha upatanishi na pande hizo mbili tarehe saba mwezi Mei.