Kuhusu Afrika Kusini

Jamhuri ya Afrika Kusini, iko katika ncha ya kusini kabisa mwa bara la Afrika. Nchi hiyo ina ukubwa wa kilomota za mraba 1,219,912. Afrika Kusini inapakana na Namibia, Botswana, Zimbabwe na Msumbiji kwa upande wa kaskazini, na Swaziland upande wa mashariki. Hata hivyo Afrika Kusini imeizunguka pande zote nchi ya kifalme ya Lesotho.

Afrika Kusini ina zaidi ya watu milioni 47 katika majimbo tisa ya nchi hiyo. Majimbo hayo ni Eastern Cape, Free State, Gauteng, Kwazulu-Natal, Limpopo, Mpumalanga, Northern Cape, North West na Western Cape. Northern Cape ndio jimbo kubwa zaidi, lakini lina idadi ndogo zaidi ya watu, huku jimbo dodo la Gauteng likiwa na msongamano mkubwa wa makazi ya watu.

Image caption Sehemu ya mji wa Cape Town

Afrika Kusini ni nchi ya kidemokrasia, ambapo rais ndio mkuu wa nchi. Mgawanyo wa utawala uko wazi nchini humo, bunge linaongozwa na spika wa bunge, shughuli za nchi za kiutawala zikiongozwa na rais na baraza la mawaziri (ambao pia ni wabunge) na idara ya sheria ikiongozwa na mwanassheria mkuu. Katiba ya Afrika Kusini hata hivyo ndio sheria kuu ya nchi ambayo ina uwezo wa juu kuliko idara zote za serikali. Wananchi wa Afrika Kusini wanajivunia katiba yao na inaonekana kuwa moja ya katiba iliyopiga hatua kubwa na iliyo huru duniani.

Afrika Kusini ina miji mikuu mitatu: Cape Town ambao ni mji mkuu wa shughuli za bunge, Pretoria - shughuli za kiutawala wa nchi na Bloemfontein kwa ajili ya shughuli za kisheria. Serikali nayo imewawanywa kwa sehemu kuu tatu: Taifa, jimbo na serikali za mitaa.

Nchi hiyo ina mandhari asili ya kpendeza, ikiwemo nyika, milima, maziwa, bahari na miji ya kisasa ya kupendeza. Kuna hifadhi ku mbili za taifa, ya kwanza ikiwa ni mbuga ya wanyama ya Kruger na maeneo manne ya kiasili yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa. Milima ya uKhahlamba/Drakensburg ni maeneo ya kihistoria kwa sababu ya michoro iliyoachwa na watu wa kabila la San, walioishi katika eneo hilo kwa miaka 4000.

Kitu cha thamani ambacho Afrika Kusini inacho, ni wananchi wake, na hiyo ilisababisha Askofu Mkuu Desmond Tutu kulipa taifa hilo jina la 'Taifa la upinde wa mvua' (Rainbow Nation). Hii ni kutokana na mchanganyiko wa utamaduni, historia na lugha nchini humo.

Image caption Askofu Mkuu Desmond Tutu

Kuna lugha 11 rasmi zinazotambuliwa nchini humo, lakini Kiingereza kinatumika katika ishara za barabarani, katika mahoteli, biashara na shughuli za kiserikali. Afrika Kusini iko nyuma saa moja ikilinganishwa na saa za Afrika Mashariki.

Licha ya kuwa na mcganganyiko mkubwa wa kitamaduni na lugha kadhaa, taifa hilo linapenda sana michezo, na hasa rugby, kriketi, golf, kuogelea, riadha, na bila shaka, soka. Soka pia hujulikana kama 'diski'.

Kwa ujumla hali ya miundombinu nchini Afrika Kusini ni nzuri sana, na kusafiri kutoka mji mmoja kwenda mwingine ni rahisi. Michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, imechochea kufanyiwa marekebisho zaidi ya miundombinu na serikali ya Afrika Kusini imewekeza zaidi ya Rand bilioni tisa.