Interyaichapa Barcelona, yatinga fainali

Inter Milan chini ya Jose Mourinho, ilicheza mechi ya kujihami kuizuia Barcelona isifunge zaidi ya goli moja na kufuzu kucheza fainali ya kombe la ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya kwenye mechi iliyochezwa Nou Camp, himaya ya Barcelona.

Image caption Mourinho ameiwezesha Inter kufika fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1972.

Wakicheza ugenini na faida ya ushindi wa 3-1 walioupata nyumbani, Inter walilazimika kucheza kwa zaidi ya saa moja wakiwa na wachezaji 10 baada ya Thiago Motta kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumfanyia madhambi Sergio Busquets.

Lakini Barca walishindwa kufungua milango ya Inter mpaka mkwaju wa Gerard Pique ulipohitimisha mpambano huo mkali.

Historia

Baada ya hapo shambulio la Bojan Krkic lilikataliwa na mwamuzi, na Inter walifanikiwa kulinda idadi yao ya magoli kuweza kucheza fainali ya ligi ya vilabu bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 1972.

Miamba hiyo ya Italia, sasa itachuana na Bayern Munich katika fainali itakayopigwa uwanja wa Bernabeu tarehe 22 Mei wakati Mourinho atakapoongoza timu yake kuwania taji hilo kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 40.

Jitihada za Barcelona kuwa timu ya kwanza kutetea kombe hilo, ziliisha kwa uchungu kutokana na Inter Milan kucheza kwa kujilinda na kuikatisha tamaa Barcelona iliyoichapa Arsenal jumla ya magoli 6-2 katika hatua iliyopita.