Bayern yaichapa Lyon kutinga fainali

Image caption Ivica Olic alifunga magoli yote matatu katika mechi dhidi ya Lyon.

Ivica Olic alifunga magoli matatu kuiwezesha Bayern Munich kufuzu kucheza fainali ya ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya itakayofanyika tarehe 22 Mei huko Madrid, Hispania.

Bayern Munich ya Ujerumani ikicheza ugenini na faida ya ushindi wa 1-0 ilioupata katika mechi ya kwanza, ilipata goli la kwanza wakati krosi ya Thomas Mueller ilipomfikia mfungaji Olic.

Baada ya hapo Lyon ilihitaji kufunga magoli matatu iweze kuwa na uhakika wa kusonga mbele, lakini matumaini yao yalizidi kufifia wakati Cris alipotolewa nje kutokana na kufanya madhambi mara mbili.

Hamit Altintop alimtengea Olic aliyekandamiza goli la pili kabla ya Philipp Lahm kutoa krosi ambayo ilimpa Olic fursa ya kukamilisha magoli yake matatu.