FKL yaidhinishwa kusimamia soka Kenya

Mpambano kati ya Nigeria na Kenya.
Image caption Matatizo ya usimamizi wa soka ya Kenya yamekuwa yakirindima kwa muda mrefu na kuathiri ufanisi wa vilabu na timu ya taifa.

Shirikisho la soka la Kenya, Kenya Football Federation (KFF) limepoteza kesi yake ya kutaka litambuliwe kuwa ndiyo mamlaka inayosimamia soka ya nchi hiyo.

Mahakama ya upatanishi wa migogoro ya michezo (CAS) badala yake imeamua kuwa wapinzani wa KFF, yaani Kenya Football Limited ndiyo ina mamlaka ya kusimia soka ya Kenya.

Mgogoro wa uongozi wa soka umekuwa ukirindima kwa zaidi ya miaka sita, baada ya shirikisho la soka duniani, Fifa, kuifungia KFF kwa maelezo kuwa serikali ilikuwa ikiingilia uendeshaji wake.

Mwaka 2006, Fifa na KFF zilifikia makubaliano na serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa chama cha soka kitaendelea kuendeshwa bila kuingiliwa na serikali.

Pande zote mbili zilihasimiana miezi kadhaa baadaye huku Fifa ikisema KFF na serikali ya Kenya hazikuheshimu makubaliano hayo.

Hatimaye kundi la wasimamizi wa soka waliunda shirika jipya, KFL ambalo lilitambuliwa na Fifa mwaka 2008.

Hatua hiyo ilisababisha KFF kuishtaki Fifa kwa kushindwa kuitambua na Fifa kuunga mkono kampuni iliyoanzishwa kibiashara, Football Kenya Limited (FKL), inayoendeshwa na watu watatu.

Lakini katika uamuzi wake siku ya Jumanne, CAS ilisema inapuuza rufaa ya KFF na kuiagiza KFL kuendelea kuwa shirika linalotambuliwa kusimamia maswala ya soka ya Kenya.