FC Twente mabingwa Uholanzi

Steve McLaren kocha wa FC Twente
Image caption Steve McLaren kocha wa FC Twente akibeba kikombe baada ya timu yake kushinda.

Klabu ya Fc Twente imetwaa taji la ubingwa wa Uholanzi kwa mara ya kwanza katika miaka 45 ya historia ya timu hiyo ambayo inafunzwa na Steven McLaren aliyewahi kuifunza timu ya taifa ya England.

McLaren, alifukuzwa kazi ya kocha wa England mwaka 2007, ni kocha wa kwanza wa kiingereza kushinda taji la mojawapo ya ligi kubwa barani Ulaya tangu Sir Bobby Robson akiwa na Porto mwaka 1996.

Twente walienda kucheza dhidi ya NAC Breda katika siku ya mwisho ya ligi wakiwa na pointi moja zaidi ya Ajax inayofunzwa na Martin Jol.

Na Twente wakapata ushindi wa 2-0 dhidi ya wapinzani wao waliokuwa 10 uwanjani hata kufanya ushindi wa 4-1 ilioupata Ajax katika mpambano wao na NEC usiwe na maana.

Ajax imemaliza msimu ikiwa na magoli 86 na ilishinda mechi 14 za mwisho wa ligi, lakini Twente wamepata mafanikio kutokana na kucheza vizuri msimu mzima ambapo walishindwa mechi mbili tu.

"Leo tumeandika historia. Ni zaidi ya miujiza," McClaren alieleza kwenye tovuti ya FC Twente.