Sheffield Wednesday yazongwa na deni

Sheffield Wednesday
Image caption Idara ya ushuru yasema Sheffield imefilisika

Klabu ya soka ya Sheffield Wednesday imeandikiwa barua na idara ya ushuru ya Uingereza, kuelezea kwamba imefilisika, kutokana na kutolipa deni.

Idara ya ushuru ya Uingereza, HM Revenue and Customs, inaelezea kwamba klabu ya Sheffield Wednesday imeshindwa kulipa deni la pauni lakini tano unusu.

Hata hivyo, klabu kinasisitiza kwamba kina uwezo wa kulipa deni hilo, na kitajitetea katika mahakama kuu tarehe 11 Agosti.

Msemaji wa klabu alisema: "Tumekuwa tukishauriana na idara ya HMRC kwa wiki kadhaa. Kwa hiyo, tumesikitishwa mno na uamuzi wao".

Aliongezea: "Tungelipenda kuwaarifu mashabiki wote wa Sheffield Wednesday kwamba klabu yao haijakaribia kufilisika".

"Tunaelewa kwamba idara ya ushuru ya HMRC inajaribu kuchukua hatua kali kwa jumla dhidi ya vilabu vya soka, lakini tunahisi kwamba hatua hiyo haikufaa, na huenda ikazuia hisia zisizofaa kuhusiana na hali ya kifedha ya klabu".

Klabu ya Sheffield Wednesday ni kati ya vilabu miongoni mwa vile vilivyo katika daraja nne bora zaidi, kukumbwa na matatizo ya kifedha.

Portsmouth ilikuwa klabu ya kwanza ya ligi kuu ya Premier kufilisika mwezi Februari, kutokana na deni la karibu pauni milioni 70.