Mano Menezes ndiye kocha mpya wa Brazil

Mano Menezes
Image caption Kocha mpya wa Brazil

Kocha Mano Menezes wa timu ya klabu ya nyumbani, Corinthians, sasa ndiye kocha mpya wa timu ya taifa ya soka ya Brazil.

Shirikisho la soka nchini Brazil, CBF, limethibitisha kwamba Menezes ameikubali kazi hiyo.

Shirikisho hilo la CBC lilimtaka Menezes, mwenye umri wa miaka 48, kuifanya kazi hiyo, baada ya mtu waliyemchagua kwanza, Muricy Ramalho, kushindwa kuikubali.

Klabu ya Fluminense ilimtaka Ramalho kuzingatia mkataba wake hadi utakapokwisha, na kuendelea hadi mwaka 2012.

Katika miaka ya hivi karibuni, Menezes ameweza kuiongoza klabu ya Corinthians, na kabla ya hapo Gremio, kutoka katika daraja ya kwanza, hadi ligi kuu.

Brazil, ambayo itakuwa ni mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, ilikuwa ikimtafuta kocha mpya, baada ya kumfuta kazi Dunga.

Hii ni kwa kuwa Brazil iliondolewa katika robo fainali, katika mashindano yaliyopita ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, mapema mwezi huu.

Menezes mwenyewe amesema; "nimeikubali kikamilifu kazi hiyo na kwa fahari kubwa, kuifundisha timu ya taifa".